Social Icons

INSPIRATION (SHARE YOUR STORY)


PROMISING ENTERPRENEURS.....PROMISING FUTURE.....



Hi all ,

This will be a new section kwenye blog tutakutana na watu mbalimbali wanaojihusisha na ujasiriamali/biashara/kilimo/na shughuli mbalimbali za maendeleo. Watatuelezea safari yao kimaendeleo, wametokea wapi, wako wapi na wanaelekea wapi. Wamepitia changamoto gani na wamefikaje hapo walipo leo. 




Nakaribisha maoni/mawazo/ushauri wa nani awe hapa ili niweze kumtafuta na ajibu maswali yetu.  Pia nakaribisha wale ambao wangependa kuwa mentor wa aina yoyote ile mfano wewe ni mtaalamu wa kompyuta na kuna mwanafunzi anasomea kompyuta chuoni angependa kujua zaidi kuhusu shughuli zako za kila siku ili afanye maamuzi sahihi ya career yake. Pia nakaribisha wale ambao wangependa kupata mentors kwenye fani mbalimbali za kimaendeleo. 


Pia tutajifunza mbinu mbali mbali za kufanya interviews, kutafuta kazi, kujiingiza kwenye ujasiriamali na kutambua unapendelea nini maishani. Je, unajua una wito gani maishani? Jifunze hapa ili tuweze kujitambua zaidi na zaidi

Asanteni sana......



UNA JAMBO LA KUTUAMBIA/KUTUKUMBUSHA

 
 
Did you see the light at the end of the tunnel and get through?
 
Unahisi mapito yako kimaisha au kimahusiano yanaweza yakawasaidia wengine? Tungependa kusikia kutoka kwako tuwasiliane Mwanadada1006@gmail.com
 
Wengi wanaumia wenyewe wakihisi hakuna atakayewaelewa huwezi jua story yako inaweza ikamsaidia mwingine kuona kuwa sio yeye peke yake na akajifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto
 



KWA WASOMI WA KIZAZI CHANGU
Na: Mtumishi Conrad Conwell




KWA WASOMI WA KIZAZI CHANGU................
Elimu ya madarasani sio mbaya,-ni nzuri kabisa! Tatizo lake ni kuwa ime-specialize kumfundisha muhitimu jinsi ya kutatua matatizo ya wengine huku ya kwake yakidoda. Ndio maana sio ajabu kuona muhitimu wa "Community Development" akiwa anafanya vizuri "ajirani" lakini yeye binafsi hana maendeleo. Wengine wamesoma "Business & Finance"; na ukiwakuta "ajirani" wanajitahidi kweli kweli kufanya biashara za "waliowaajiri" lakini hawana jeuri ya kuanzisha biashara zao japo kufungua mabanda ya chips tu! Wapo wale wanaosoma, "Bachelors of Counciling & Psychology"; ukiwakuta wanavyoshauri ndoa, migogoro na matatizo ya wengine; utawapenda! Sasa njoo kwenye maisha yao binafsi; utawahurumia! ndoa zinawasumbua, mahusiano yanawahenyesha, matatizo hayawaishi kila kukicha. 

Ndio maana hekima inatueleza kuwa: Ukishapata vyeti vyako, usibweteke; chukua hatua nyingine ya kujifunza kutoka kwa wanaotatua matatizo yao. Hili utalipata kwa ama kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, kusoma vitabu vya waliojaribu na kufanikiwa ama kufanya yote mawili. Elimu ya maisha ni zaidi ya vyeti tunavyopata madarasani







MTANZANIA ZINDUKA.....
Na: Meshack Maganga-Iringa.


Nimemaliza kusoma kitabu cha ‘Success Principles’ Kilicho andikwa na Jack Canfield, kwenye kitabu hiki nimejifunza kwamba, ukitaka kufanikiwa kwenye mambo yako lazima utambue kwamba  wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa maisha yako, mazingira, mifumo, familia na vikwazo vyovyote duniani visiwe sababu ya kuutuliza utu wako. Unazo nguvu zaidi ya nguvu zilizo nje yako za kuwa unavyotaka, kulingana na jinsi ulivyojaliwa. Vipo vitu vinavyoweza kukuzuia hata kukumaliza lakini ni uamuzi wako kusimama kidete kwaajili ya maisha yako na kuonyesha nguvu zilizo ndani yako au kukubali kumalizwa bila ubishi wowote. 

Mwanzoni mwa mwaka huu,  nilibahatika kusoma  makala ya mwandishi maarufu Freddy Macha kwenye gazeti la Mwananchi yenye kichwa ‘Maisha Bongo,Majuu hali moja’. Kwenye makala yake Freddy Macha alilezea waziwazi kwamba wapo baadhi ya vijana wa kibongo ambao huota kwenda kuishi ‘majuu’ bila kujua kwamba huko maisha ni magumu kuliko hata bongo,na kwamba, popote pale unapoishi utawakuta watu wakilalamika na kusema kuwa afadhali kwenda mahali pengine. Kisha akaenda mbali kwakusema kuwa, ukijua na kutambua la kufanya na namna ya kumudu maisha,unaendelea na mapambano,kwa sababu kanuni kuu ya  uhai ni harakati.

Kwenye makala zangu mabalimbali mimi na Albert Sanga, tumekuwa tukiwaelezea watanzania wenzetu juu ya kuwekeza kwenye kilimo cha miti, mboga na matunda na ufugaji wapo walio elewa na wapo wanaolalamika umbali wa masaa mawili kutoka sehemu wanayoishi mpaka mashambani. Na wapo wanaoona kwamba kilimo ni kazi za watu duni, walioshindwa shule, nk. Na wapo ambao wameamua kuwa wanaharakati wa kusifia maisha ya wacheza mpira wa ligi za ulaya na kupoteza muda vijiweni.

Kwenye makala yake, Albert Sanga yenye kichwa WATANZANIA NA ARDHI alisema,  Jambo jingine linalotumaliza watanzania ni kutokuwa na maono ya muda mrefu. Wengi wetu tunataka mambo ya papo kwa papo, hatupendi kuangalia mambo ya vipindi virefu mbele. Mfano mzuri ni katika hili la uwekezaji katika ardhi.

Mtu anaona ni kupoteza fedha kununua shamba leo ambalo pengine linaweza kuja kutumika miaka ishirini huko baadae. Mtu anaona ni kama kupoteza fedha kupanda miti leo ambayo atakuja kuivuna miaka saba ama miaka kumi ijayo.
Wasichokumbuka wengi ni kuwa unachopuuza kufanya leo kwa gharama ndogo miaka ishirini ama kumi ijayo hutakuwa na uwezo wa kukifanya hata kama ukitamani.
Kwa bahati nzuri zaidi, wataalamu wa masuala ya utambuzi na mafanikio na wajasiriamali maarufu hapa Tanzania na kwingineko duniani kama John Gray, Vincent Peale,   Robert Kiyosaki, Donald Trump, Jack Canfield, Anthony Robbins na wengine, wanabainisha vigezo ambavyo vinaweza kumfanya mtu kutabiri kama maisha yake yatakuwa ni ya kushindwa hadi mwisho au yatakuwa ni ya mafanikio.

Mwana mama Rhonda Byrne kwenye kitabu chake cha ‘The Secret’ ameeleza kwamba, kama mtu akiwa anaamini kwamba kuna watu wengine wa aina fulani mahali fulani, ambao ndio peke yao wanaoweza kufanikiwa na kufika juu kwenye ngazi ya kimapato, mtu kama huyo hawezi kamwe maishani mwake kuja kutoka kwenye lindi la umaskini.
Rhonda, ambae aliishi maisha ya hali ya chini nayakutisha,anafafanua kwamba, mtu akiwa na mtazamo huo, hawezi kutoka kwenye lindi hilo kwa sababu juhudi zake ambazo zingemfikisha mbali zinakuwa tayari zimewekewa mipaka na imani hiyo, kwamba yeye hahusiki  katika kufanikiwa, bali kuna wengine ambao ni Mungu mwenyewe  anayewajua na aliyewateua. Kwa kufikiri hivo, juhudi yake kubwa  katika kutafuta itakuwa ni ile ya kumfanya asife tu kwa njaa na siyo kuvuka hapo. Kama ujuavyo, tunapoamini kuhusu jambo Fulani, mawazo yetu hutusaidia kulifikia jambo hilo.

Kuna mwandishi wa kitabu cha Jitambue enzi zile 2006 nikiwa bado mwanafunzi wa sekondari aliwahi kuandika kwamba, ‘Hata kama “fuko la fedha” litadondoshwa miguu mwetu tutalipiga teke na kuliambia “mimi sikuandikiwa kupata bwana, kuna wenyewe, hali kama hii hujitokeza mara nyingi sana maishani mwetu.”
 Tunakabidhiwa dhamana kubwa ambayo ingetusaidia sana maishani mwetu, lakini tunacheza nayo hadi inapotea kwa sababu tu hatuamini kwamba utunastahili kuitumia kufika juu. Tunaziona nafasi za kusonga mbele, lakini tunaamini kwamba, hatustahili kuzitumia.

Fursa zikija waziwazi kabisa, tunajifanya hatuzioni kwa kutafuta visingizio mbalimbali ili tusizitumie, kwa sababu tu, tumeamini kwenye mawazo yetu kwamba, sisi hatustahili.
Ni vigumu kugundua kwamba nafasi au fursa hizo zimekuja kwa sababu tayari tumejifungia njia kuelekea mafanikio. Wengine kwa bahati mbaya wanaweza kuona na kubaki wameshangaa ni kwa nini tushindwa kuinuka katika mazingira tuliyomo.
Mtu anapoamini kwamba hawezi, anayaambia mawazo yake ya kina yamsaidie kumfanya ashindwe zaidi kwenye kila jaribio analofanya. Badala ya kufanya juhudi kujisaidia ili amudu, hujipweteka kwa kuamini kwake kwamba hata kama atafanya kitu gani, kamwe hatamudu. Siyo rahisi kwa mtu mwenye mawazo ya aina hii kuweza kufanikiwa maishani.
Kuna watu ambao kwa sababu ya kukosa kile ambacho jamii inakiona kuwa ndiyo ufunguo wa mafanikio, huwa wanaamini kwamba hawawezi kufanikiwa au kufanya vizuri maishani kama hao ambao wanacho. Kwa mfano, kwa kukosa elimu, ujuzi au utaalamu fulani, watu wengine hujihesabu kama wanyonge. Huchukulia kwamba ni wale tu wenye elimu, ujuzi na utaalamu fulani ndiyo wanaoweza au wanaotakiwa kufanikiwa.

Bila shaka umeshawahi kusikia au hata wewe mwenyewe kusema, “Si wamesoma bwana’ ndiyo wanaojaliwa, sisi ambao hatuna elimu kazi yetu itakuwa ni kuwatumikia. Kauli kama hizi zina chimbuko lake mbali sana, pengine katika malezi yetu. Wazazi kwalizoea au wamezoea kuwaambia watoto wao, “Usiposoma kazi yako itakuwa ni kuwabebea wenzako mizigo, unafikiri pesa inaokotwa, nk.  Kwa bahati mbaya mtoto aliyelishwa “sumu” (‘EARLY CHILD PROGRAMMING’) hii anaposhindwa shule, huamini kwamba yeye atabaki kuwatumikia wengine tu.

Tunapoamini kwamba kwa sababu hatuna elimu ya kutosha na pengine ujuzi au utaalamu fulani, hatuwezi kufika juu kwenye mafanikio, tutakuwa tunatafuta kufulia( ama vifafa vya kiuchumi). Moja ya vigezo muhumu vinavyoweza  kutufikisha kwenye mafanikio ni kuamini kwetu kwamba tunaweza kufika huko. Tunapokuwa hatuna imani kwamba tunaweza kufika huko hujifungia njia wenyewe.

Baadhi yetu kuwa tunaamini kwamba tuna mikosi, balaa au nuksi napengine laana ambazo zinatuzuia katika kufikia malengo yetu. Tunaamini hivyo kiasi kwamba hata tukifikia karibu kabisa na mafanikio huwa tunajiambia ni kazi bure, tutaporomoka tu. Na kweli kwa kuamini hivyo hujikuta tukiporomoka kila tukifika karibu na kufanikwa au kufikia malengo. 
Kinachotokea ni kwamba, kwa kuamini kwetu kuwa tunamkosi, balaa, laana au nuksi, huwa tunatenda kwa mkabala huo wa kinuksi au kibalaa na kimkosi, ambapo matokeo yake ni kujikwamisha. Watalaamu wa elimu ya mafanikio wanaeleza kwamba tunapoamini kuwa tuna mkosi au nuksi huwa tunayashauri mawazo yetu ya kina kutusaidia kuendelea kuwa katika hali hizo (Niliwahi kufafanua zana hii nilipoandika makala ya BINADAMU NI ZAIDI YA MWILI WAKE). Ndiyo maana siyo rahisi  kukuta mtu anayeamini katika nuksi akiondoka katika hali hiyo.
Tufanyeje basi, kama ni kweli kimapato tuko hoi napengine tunachoweza ni kupata riziki yetu ya kila siku tu? Pamoja na kwamba mengi yameelezwa  tayari kwenye mada nyingine, bado tunaweza kukuambia, tunachotakiwa kufanya ni kujenga imani ya kumudu. Kamwe hatutakiwi kabisa kujiambia tulipofikia ndipo basi, hatuwezi kupanda zaidi.

Yupo mjasiliamali fulani,ni dada mpambanaji (Elizabeth Samoja) kwenye ujasiriamali alipata kuandika hivi, maisha ya kijana wa kitanzania aliyechagua kuishi Dar es salaam baada ya kumaliza masomo yake ya chuo kikuu huwa hayaelewiki,(ingawa kwa mtazamo wake yanaeleweka) utashangaa kijana huyu anapomaliza chuo anaanza zungusha cv ndani ya bahasha ya kaki,mtaa kwa mtaa,jingo kwa jingo,atapata kazi kampuni ya simu,au bank,au kampuni ya bia, atapanga chumba mitaa ya  sinza, wengine huchukua mkopo  na nunua gari aina ya  vitis,corora,corona, opa, ama gari lolote lisilozidi milioni  kumi, ataoa amakuolewa,atafanya shopping Mr Price, mjanja mwingine atakopa hela za kwendea ‘sendoff’ na wengi wao wakijitahidi hununua mariedo, atavaatai kubwa na kuonekana smart, ataenda club, kuponda raha...

Ukiungalia mlolongo huu vizuri,shughuri nyingi hapo kati zote zinachukua pesa mfukoni mwa ila chanzo cha pato lako ni kimoja tu(ajira), kwa kifupi wewe ni mtumiaji tu....kutoboa kimaisha kwa kufuata mpango huu ngumu sana................

Imefika hatua mpaka mabenki wamejua watanzania si entrepreneurs na investors wanapenda magari ya bei chee,na akijitahidi basi apate nyumba bunju,mbagala,au kitunda.....ndo maana mikopo mingi ya benki wanatangaza kwa kuonyesha nyumba ama gari....maana huko ndo kwenye urahisi na kuna soko na wateja wakubwa maarufu kama ‘victim society’ market. Mtanzania Zinduka......

Usiseme hakuna pesa, pesa zipo nyingi sana, fursa za kumwaga, nina mshangaa huyu mhitimu wa chuo kikuu akiwa mtaani asijue cha kufanya badala yake anaingia kwenye mitandao ya kijamii kama ‘Face
book na kuanza kumwaga lawama kibao,jiulize umefanya nini,kwani ulikuja duniani ili ubebwe na serikali? Kwa sasa Tupo watanzania milioni 44 wote tukisubiri kubebwa tutakuwa taifa la aina gani hili?
meshackmaganga@gmail.com  0767 48 66 36/ 0713 48 66 36.



CHAGUA KUFANIKIWA - MESHACK MAGANGA



MAISHA NI VITENDO NA SI NDOTO PEKEE, NDOTO NI MWANZO TU WA MAISHA

Meshack Maganga-Iringa.
Katika makala zangu huko nyuma nilipata kuandika makala moja niliyoipa kichwa cha KWENYE UJASIRIAMALI NG'OMBE WA MASKINI HUZAA nilizungumzia na kukanusha juu ya imani potofu isemayo 'NG'OMBE WA MASKINI HAZAI', nilisema kuwa, kwenye ujasiriamali ni kinyume chake, kwamba Ng'ombe wa maskini anaweza kuzaa tena mapacha. Nilielezea kwa kirefu jinsi ambavyo baadhi tunapokuwa tumetafuta mitaji, na kuhangaika hapa na pale na ikatokea muda mwingi umepita bila kufanikiwa huwa tuna kata tama na kuanza kutamka maneno na methali kama hiyo hapo juu.

Nilieleza kwamba kuna kanuni vichwani mwetu na tunaweza kuitumia katika kutupatia hamasa ya kuwa wajasiriamali wakubwa na bora kuliko wote hapa duniani.Leo nianze kwakusema kwamba, binadamu ana mambo matatu muhimu ambayo anaweza kuyaendesha au yakamwendesha kichwani kwake, moja ni fikra zake au mtazamo(thoughts you think),mbili ni taswira anazozijenga kichwani kwake(image you visualize) na tatu ni vitendo vyake (the actions you take).Sisi binadamu tunawajibu wakuhakikisha tunaleta maendeleo katika maeneo tunayoishi kwa juhudi zetu binafsi. Ni kweli tumesikia na kujifunza mengi katika dunia lakini maana ya maisha iliyo halisi na ya kweli ya mwanadamu mhusika hutoka ndani ya binadamu mwenyewe. Kila mwanadamu anao ukweli wa maisha yake ndani yake.

Mambo yote tunayoyaona duniani, ugunduzi, vitabu, miziki, filamu na kila kitu kilichopo duniani kilichosababishwa na mwanadamu asili yake ni ndani ya binadamu na si nje. Ndani yako mwanadamu kuna maajabu, ndani yako kuna hazina ya maisha, vipaji, talanta na habari njema ya maisha yako.

Kutokana na upekee ulionao duniani, huna mshindani, mshindani wako ni wewe mwenyewe.Historia ya dunia inaonyesha kuwa wanadamu walio wengi duniani wanafichwa mambo ya ukweli na makubwa kuhusu uwezo wao.
Toka enzi za wajasiriamali tunaowasoma katika historia akina Adam Smith, kipindi cha viwanda na utumwa wanadamu wengi, waliishi chini ya viwango kwa kutumika kama mashine zinazoweza kubadilishwa wakati wowote, hii imekuwa sababu kubwa ya binadamu wengi kutokujua ukweli wa vipawa ndani yao na hata kutojiamini kabisa.
Vilevile Kutokana na mabadiliko ya maisha, karne hii ya 21 inatabiriwa kuwa karne ya vipawa na maajabu ya ndani ya mwanadamu kwani imedhihirishwa na baadhi ya watu wa kawaida sana ambao wameweza kugundua mambo mengi kwa kutumia vipawa vyao.

Tunaishi katika dunia ambayo ni rahisi kubebwa na misukumo ya nje na wengi hawaamini ukweli huu kuwa kila mtu ana kipaji, kila mtu ana habari njema ya ndani yake hii ni kwasababu wengi wameshawishiwa na mifumo ya dunia na maisha ya wanadamu wengine na kujikuta kuwa wanaishi si kama wao bali kama nakala.
Watu wote wenye mafanikio duniani, ambao huonekana kana kwamba wamebarikiwa hutafuta maana ya wao kuwa wao, uwezo wao wa kipekee na kutumia upekee walionao na kuishi maisha yao kimafanikio watakavyo wao.

Dunia hii inayo nafasi kwa mwanadamu ambaye anatafuta maana ya maisha yake mwenyewe, haijalishi umezaliwa katika familia ya aina gani bali ukikubali ukweli kuwa unayo hazina ya maisha ndani yako basi maisha yako yatapata maana.
Unacho kipaji ndani yako.Hakuna mwanadamu ambaye hakuumbwa na kitu ndani yake, Mungu hakuumba takataka duniani, Mungu aliumba mwanadamu mwenye hazina ndani yake. Kila mwanadamu anao uwezo wa kipekee na kiasili aliojaliwa na Mungu ambao bila yeye hakuna ukamilifu. Uliletwa duniani ili ukamilishe upekee wako. Wewe ni ukamilifu wa dunia, kuishi kama nakala haina tofauti na kuishi kama marehemu anayetembea.
Unaweza usiwe na uwezo kuanzisha biashara ya mgahawa au ya daladala lakini ukawa na uwezo wa kuimba na kutunga nyimbo za kila aina hivyo ukawa mjasiriamalia katika kanda ya mziki iwapo una uwezo wa kuchekesha basi fanya ujasiriamali katika kipengele cha ucheshi kama jamaa wa futuhi.

Wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheke, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia icheze,wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia itembee, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia ifikiri, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia isikilize radio,TVs na muziki, wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia ing'are na mengine mengi unayoyajua na ambayo mpaka sasa hatujayajua bado lakini yamo ndani yako. Aidha wapo walioletwa duniani ili kuifanya dunia iwe na mitandao tunayoiona sasa hivi.

Dunia hii inakuhitaji wewe kama wewe, na mafanikio yako duniani yanakutegemea wewe kama wewe. Hata kama usipokubali ukweli wa uwezo wako wa ndani, haitaondoa maana ya ukweli ulio ndani yako. Kumbuka kuwa utamu wa maisha duniani ni matumizi ya kipaji chako na kusikiliza sauti ya ndani.Ulipewa vipaji ili uvitumie duniani katika biashara,kazi,sanaa,uongozi,ujuzi,masomo na mengine.

Bila kujionea aibu mwenyewe, na kujitafuta na kujiuliza kasoro zako ulizonazo na jinsi ya kuzizuia au kuzipunguza, tafuta kujua mazuri ya kwako huku ukitafuta kuongeza mengine. Ukiona Kama kuna kitu kinakufurahisha duniani, usiogope kujaribu, jaribu, jaribu tena ipo siku utagundua wewe ni mzuri wapi.
Sikiliza sauti za dunia lakini sikiliza sana sana sauti yako ya ndani kwani ndiko kutokako chemchem ya uhai wa maisha yako. Jifunze kujiuliza, wewe ni nani? Umetoka wapi? Una nini cha kujivunia duniani? Unataka dunia ikukumbuke vipi? Je uko tayari kuja duniani kama moshi na kuondoka kama moshi, usikumbukwe? Nini unaweza zaidi ya mwingine? Ni nini madhumuni yako duniani?

Kumbuka kuwa wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa maisha yako, mazingira, mifumo, familia na vikwazo vyovyote duniani visiwe sababu ya kuutuliza utu wako. Unazo nguvu zaidi ya nguvu zilizo nje yako za kuwa unavyotaka, kulingana na jinsi ulivyojaliwa. Vipo vitu vinavyoweza kukuzuia hata kukumaliza lakini ni uamuzi wako kusimama kidete kwaajili ya maisha yako na kuonyesha nguvu zilizo ndani yako au kukubali kumalizwa bila ubishi wowote.

Vipo vitu vingi vinavyoweza kukuchanganya. Lakini ni uamuzi wako kukubali kuchanganywa na kuishi maisha ya bora liende au ili mradi kumekucha mpaka unakufa bila maana au kuamua maisha yako na kusema ama zangu ama zao nitakuwa vile ninavyotaka maishani.
Kumbuka kuwa dunia haina huruma kwa mwanadamu aliyekubali kumalizwa, vumilia, jiamini, Jipende, jiendeleze, jikaze, jionyeshe, jitafute mwenyewe, jikubali na mwisho wa siku dunia itakukubali tu hata kama kuwe na nguvu zozote mbele yako.
Kumbuka kuwa dunia hii itaendelea kuendeshwa na hata kutengenezwa na binadamu wenye uelewa mpana wa nguvu iliyo ndani yao na si wababaishaji na wenye maisha ya maridadi.Wanadamu wote walioweza kufanikiwa.

Juzi kuna rafiki yangu anaye soma katika moja ya vyuo vikuu hapa Iringa, alikuja ofisini kwangu na kuniuliza "unanisahuri nikimaliza masomo yangu ni fanye kazi katika kampuni gani"? mwanzo nilishangaa msomi wa chuo kikuu akiuliza swali hilo,nilitambua kwamba kuna umuhimu wa wanafunzi kufundishwa somo la utambuzi ili wafahamu vipaji vyao.Hasa kwa vile watanzania hawana utamaduni wa kujisomea makala na vitabu vya utambuzi na maarifa na siyo wanafunzi tu,ni pamoja na walimu wao na wahadhiri wao na viongozi kwa ujumla, anaye pinga aniambie.

Tunachoweza ni kulaumu watu wasiohusika katika maisha yetu magumu, kuwa wanaharakati wa mambo yasiyotuhusu,kutoa maoni yasiyo na maoni na kuchambua timu za ulaya na kuelezea mchezaji fulani analipwa kiasi gani cha mshahara.Ni lini umewahi kaa nyumbani kwako au kwenu na ukatumia muda wako kuchambua vipaji vyako? Ambavyo ungevitumia katika maisha yako na jamii inayokuzunguka?
Kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wanajijua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe.

Maisha ya mafanikio duniani ni haki ya kila mwanadamu. Hakuna binadamu aliyeletwa duniani kuja kushuhudia wengine wakifanikiwa huku yeye akiwa katika umaskini siku zote. Kila mwanadamu mwenye pumzi anayo haki, nafasi, uwezo na uchaguzi wa kuwa anavyotaka kulingana na maana ya mafanikio atakayotengeneza na mwenyewe.
Ni kweli tunaishi katika dunia yenye utofauti kimafanikio wapo wenye mafanikio makubwa, wapo maskini na wale wenye maisha ya kawaida. Lakini kwa pamoja yatupasa tufahamu kuwa, kila mwanadamu anao uwezo wa kufanikiwa.
Na zaidi ni kuwa kila mtu anao uchaguzi wa kuamua maisha yake, lakini angalizo ni kuwa mtu yeyote aliyeweza kufanikiwa ametambua kuwa , kuna vichangizi vya
mafanikio / success ingredients.

Unachopaswa kutambua ni kuwa, hali ya maisha uliyonayo sasa si kipimo cha mafanikio yako ya baadaye, unaweza kuwa vyovyote kimafanikio kulingana na utakavyochagua mwenyewe. Ni muhimu kuyajua maisha Kwa kujua vipaji na vichagizi hivyo ni kama vifuatavyo:
Mwanadamu anayejua dhumuni lake duniani huishi maisha ya maana. Hatukuja duniani kuwepo tu bali kuishi kimafanikio huku tukijua kwanini tunaishi. Ukijua ni kwanini unaishi hutakubali kuishi kiholelaholela huku ukisubiri muda wako wa kuishi duniani kuisha.
Dhumuni la wewe kuwepo duniani ni kuishi maisha yenye madhumuni, maisha yenye mafanikio na maisha yanayonufaisha wengine. Wanadamu wote walioweza kufanikiwa kwa kujitengenezea mafanikio wenyewe kutoka chini ni wale ambao wametambua sababu ya wao kuwa wao, wananjua ni nini wanakitaka na wanajua kuwa ili maisha yao yawe na maana lazima wafanikiwe katika hilo.Ukitaka kutengeneza maisha yenye mafanikio duniani, tafuta kujua dhumuni lako hapa duniani.

Wanadamu wote waliofanikiwa duniani waliamini kuwa wanaweza kuibadili dunia. Mwanadamu anayeyarudisha maisha yako nyuma ni wewe mwenyewe, ukitaka kufanikiwa katika lolote utakalochagua jiamini na amini kuwa unaweza. Hakuna kitu chochote kilichowahi kutokea duniani bila kujiamini.
Kila mwanadamu anayo zawadi ndani yake, zawadi hii huja kama kitu anachokipenda na kukiweza. Ndani ya mwanadamu vipo vipawa na uwezo wa ajabu wa kuishi maisha ya mafanikio. Kila mtu ana kitu anachopenda, kinachoweza kutumika na kuendelezwa na kuleta mafanikio.
Dunia ya sasa ni dunia ya wanadamu wanaojua ni kitu gani wanaweza. Wapo wanaopenda kuwa madaktari, wapo wanaopenda kuwa waimbaji nk. Kila mtu ana kitu anachopenda kinachomfanya acheke akiwa duniani. Tafuta kitu unachokipenda na kiendeleze, kitakuletea mafanikio.

Maisha ni vitendo na si ndoto pekee, ndoto ni mwanzo tu wa maisha. Maisha ni kuchukua hatua na si kufikiri pekee. Maisha ya kijasiriamali ni kusonga mbele na si kupanga peke yake. Katika yote uliyochagua maishani kuwa mtendaji, usikubali kuyaishi maneno ishi matendo.
Maisha bila maarifa ni sawa na gari lisilo na mafuta. Ukitaka kutembea na kuishi kimafanikio kuwa na njaa ya maarifa kila siku. Binadamu wote wenye mafanikio duniani hawachoki kutafuta maarifa kwa kusoma vitabu, kuuliza na kujifunaza, na hata kuhudhuria mafunzo ya kuwaendeleza mara kwa mara. Maisha bila maarifa hayatembei.

Maisha yana mengi, muda mwingine yale tunayapanga hayaji kama tulivyopanga lakini yote hutokea kwasababu. Mambo yote tunayapitia katika maisha huwa ni hatua ya ukuaji kimaisha. Ukiona biashara yako inafanya vizuri tambua kuwa ni kweli biashara yako inakua, lakini ukiona biashara yako inafanya vibaya tambua kuwa uwezo wako unakua zaidi.
Nahitimisha kwa kusema kila mtu ana uwezo wa kuchagua kuwa mjasiriamali wa kipekee na yale ayatakayo maishani, Dunia ina mengi ya kuyafanya na kuna kila nafasi kwa mwanadamu yeyote anayechagua kuwa anavyotaka maishani. Chagua maisha unayotaka kuyaishi na uyaishi kweli.

Usiogope kujaribu kitu, maisha ya kuogopa kufanya kitu ni maisha yasiyo na maana. Usikubali maisha ya ukawaida na yenye usalama ambayo yatakufanya usiishi maisha makubwa unayostahili.


Siri kubwa ya watu wenye mafanikio duniani, ni kuwa hawaogopi maisha, wapo tayari kuumia kwa kuchagua maisha wayatakayo. Chagua kipengele mojawapo cha kijasiriamali unachotaka kukifanya na ukifanye kweli kwa moyo wote. Jiendeleze kila siku katika ulilochagua kiasi ambacho utavunja mipaka na kuweka rekodi yako. Chagua kufanikiwa

0 comments:

Post a Comment