Kila siku tunasikia sababu zile zile za upungufu wa walimu, uhaba wa vifaa vya kufundishia, mazingira duni ya shule, ukosefu wa maabara na maktaba hasa kwa shule za serikali. Huku shule binafsi zikiendelea kuongoza kwa spidi kubwa kila mwaka zikizitoa kileleni shule za vipaji maalum za serikali.
Tatizo hasa ni nini? Tukitafakari kwa kina na kulinganisha matokeo haya ya mwaka huu na yale yaliyopita inaonekana kabisa kuna tatizo sehemu sababu haiingii akilini kuwa karibu asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamefeli tena kwa daraja 0 (ina maana wameshindwa kupata wastani wa alama zaidi ya 20 kwa kila somo). Je wamefeli kwa kuwa hawana uelewa, mfumo wa usahihishaji umebadilika? Ukosefu wa walimu na mazingira duni ya shule wale tuliosoma shule za serikali tunalijua hilo na tulilikabili ipasavyo kwa kuongeza jitihada binafsi zaidi na zaidi kwa miaka ile.
Je, nini kifanyike? Una maoni gani au ushauri gani? Labda kuna shimo tumesahau kulifukia linameza wanafunzi kadiri muda unavyozidi kwenda? Kwanini zamani ilikuwa si kawaida kuwa na wanafunzi waliofeli kwa kiasi kikubwa namna hii? Taifa hili miaka 20 na zaidi ijayo litakuwaje? Je, tutashangazwa na maamuzi watakayofanya kipindi hiko pale watakapopata fursa za uongozi wa kijamii na kiserikali? TAFAKARI.......
0 comments:
Post a Comment