Kula kwenye meza yako hata kama unatumia hand sanitiser kila mara ni hatari kwa afya yako.....
Utafiti wa hivi karibuni umebaini kwamba,
wanawake huwazidi wanaume katika kiwango cha kujilimbikizia vijidudu vya
maradhi kwenye maeneo yanayowazunguka, ikiwa ni pamoja na meza zao za kazi
ofisini, simu zao na kompyuta wanazotumia. Vile vile makabati yao ya kuwekea
vitu ofisini au nyumbani, pamoja na vitu vyao binafsi kwa ujumla. Utafiti huo
uliofanywa na profesa Charles Gerba wa chuo kikuu cha Arizona nchini Marekani
umebaini ukweli huo kwa uwazi zaidi kuliko tafiti za awali. Gerba ambaye ni
mtaalamu wa masuala ya udongo, maji na mazingira, alichunguza na kupima zaidi
ya maofisi 100 kwenye chuo kikuu cha Arizona, New York, Los Angeles, San
Francisco, Oregon na Washington DC, katika utafiti huo uliogharimu zaidi ya
shilingi milioni 52 chini ya ufadhili wa kampuni ya Clorox.
‘Niliamini kabisa kwamba kutokana na hali ya
wanaume kutokuwa nadhifu na wasiojijali sana kama wanawake, bila shaka wangekuwa
wenye kubeba viini na vidudu zaidi vya maradhi kulinganisha na wanawake,’ alisema Gerba.
Lakini hali ni tofauti kutokana na wanawake kuwa
na kawaida ya kushirikiana kwa karibu zaidi na watu wengine na hasa watoto na
kuwa na tabia ya kupenda kuweka vyakula kwenye meza zao za kazini. Tatizo
jingine ni vipodozi. Dhana ya mwanzo ya Gerba ilitokana na ukweli kwamba meza
za wanawake siku zote huonekana nadhifu na zilizopangiliwa kulinganisha na za
wanaume, lakini mabaki japo madogo sana ya vyakula, vipodozi na mafuta ya
kujipaka ni ya kawaida kwenye meza zao na hivyo kuwa kichocheo kikuu cha
ufugaji wa viini vya maradhi..
Mikoba ya kubebea vipodozi nayo huvipatia viini
na vidudu hivi makazi ya usalama kwao, pamoja na simu na mikoba ya kubebea vitu
vyao vingine, na madroo ya kwenye meza. Vyakula vinavyohifadhiwa kwa muda
kwenye meza za maofisini navyo huvutia na kuhifadhi wadudu, na tabia hiyo ni ya
kawaida zaidi kwa wanawake kuliko wanaume. Katika utafiti wake, Gerba aligundua
kwamba, asilimia 75 ya wanawake wanakuwa na vyakula kwenye meza zao za
maofisini. Hiyo ni karibu kote duniani. Wanaobeba vyakula na kwenda navyo
ofisini ni wanawake zaidi.
‘Kwa kweli nilishangazwa na kiasi kikubwa cha
vyakula nilichokuta kimehifadhiwa kwenye meza za wanawake,’ alisema mtafiti huyo.
Kwa upande wa wanaume Gerba aligundua kwamba
sehemu ambayo husaidi kuzalisha viini vya maradhi ni kwenye pochi za wanaume
ambazo kwa kawaida huwekwa kwenye mifuko ya nyuma ya suruali ama kwenye makoti
ya suti, lakini pamoja na ukweli huo bado wanawake ndiyo wenye kuzalisha
vijidudu vya maradhi zaidi.
0 comments:
Post a Comment